Mahakama ya Haki za Binadamu Yaibuka na Babu ....Hukumu Yao Kusomwa Kesho
Wakati
mwanamuziki Nguza Viking (Babu Seya) na mwanawe Johnson Nguza (Papii
Kocha) wakiwa nje kwa msamaha wa rais, Mahakama ya Afrika ya Haki za
Binadamu na Watu (AfCHPR), imeahirisha kutoa hukumu ya maombi
waliyofungua kupinga kifungo cha maisha jela.
Babu
Seya na Papii Kocha waliachiwa kwa msamaha wa rais Desemba 9, mwaka
jana kutokana na kifungo cha maisha jela walichohukumiwa na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam Juni mwaka 2004 baada ya
kumkuta na hatia ya kunajisi na kulawiti watoto 10 ambapo walikata rufaa
Mahakama za juu na kugonga mwamba na hivyo kulazimika kukimbilia AfCHPR
wakidai haki zao zilivunjwa.
Akiahirisha
kesi hiyo Rais wa AfCHPR, Jaji Sylvaine Ore kutoka nchini Ivory Cost,
amesema wamelazimika kuahirisha kusoma hukumu hiyo hadi Ijumaa Machi 23,
kutokana na upande wa waomba maombi kutofika mahakamani.
Katika
shauri hilo Jamhuri iliwakilishwa na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Sara
Mwaipopo akisaidiana na Mwanasheria wa Serikali Mkuu Nkasori Sarakikya.
Hata
hivyo, mwanasheria Daniel Kalasha akitoa maoni yake kuhusiana na hukumu
hiyo amesema vyovyote itakavyokuwa hukumu hiyo haiwezi kuathiri msamaha
wa rais waliopata waomba maombi hao lakini walipaswa kuitaarifu
mahakama kuachana na kesi hiyo kutokana na sababu hizo.
Amesema
utaratibu ulivyo wao ndiyo walifungua hiyo kesi baada ya kuona wamepata
msamaha wa rais walikuwa wanapaswa waiandikie barua mahakama kwamba
wameshapata msamaha huo hivyo wanaomba mahakama isitoe hukumu.
“Lakini
kama hawakufanya hivyo mahakama itaendelea na kazi yake kama kawaida na
aidha itawakuta na hatia au isiwakute na hatia kwamba jambo lao
limeshapata msamaha na msamaha wa rais huwezi kuuhoji popote, hakuna
mwenye mamlaka ya kuhoji kwa sababu kile kifungo kimeshabatilishwa
tayari.
“Kesi
ingekuwa bado inaendelea msamaha ukatoka basi wakili ndiyo alikuwa na
wajibu wa kuiambia mahakama hatuna nia tena ya kuendelea na rufaa yetu
kwa hiyo kesi inakuwa imekufa.
“Lakini
hata hivyo halina uzito tena hata kama wakikutwa na hatia tayari
wameshapata msamaha wa rais ambao uko kwa mujibu wa katiba,” amesema
Kalasha.
No comments